Na Andrew Chale, Bagamoyo. / ZanziNews

Baadhi ya wahitimu wa FormIV 2018 wa Shule ya Sekondari ya Eagles
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari ya Eagles wakiwa kwenye Mahafali yao ya 10, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Oktoba 6, Mjini Bagamoyo, Mkoani Pwani.

Shule ya Sekondari ya Eagles ya Mjini Bagamoyo Mkoani Pwani imefanya sherehe za Mahafali yake ya 10 na kuzindua rasmi mfumo mpya wa menejimenti ya shule ambao utasaidia wazazi kufuatilia maendeleao ya Watoto wao kwa ukaribu zaidi.

Akizundua mfumo huo sambamba na kutoa neno kwa wahitimu 71 wa kidato cha Nne wa shule hiyo mwishoni mwa wiki Oktoba 6,2018, Mgeni rasmi Mkaguzi na mdhibiti wa elimu bora Wilaya ya Bagamoyo Bwana. Davis Moye amewataka kuzingatia maadili sambamba na kujiandaa vyema kwa mitihani yao hiyo ya kuhitimu.

Akitoa neno kwa wahitimu hao: “Mjiandae vyema na mtafanya vizuri kwenye mitihani yenu. Pia niwapongeze kwa Eagles kuja na mfumo huu ambao utasaidia Wanafunzi na walimu kufanya mambo kifanisi zaidi.” Ameeleza Bwana Davis Moye.
Hata hivyo, amewataka Wazazi kufuatilia na kuwa karibu na watoto wao ili kubaini mapungufu kwa hatua ya kuyatatua.

Nae Mwenyekiti wa Bodi wa shule hiyo, Bi. Eva Fumbuka amejivunia kufanya vizuri kitaalum huku lengo kwa shule hiyo ni kuwa shule bora Kitaifa.
“Eagles mwaka 2006, ilikuwa ya kwanza kwa wavulana tupu kwa Wilaya ya Bagamoyo. Leo mahafali ya 10, matamanio yetu ni kufikia nafasi za juu zaidi kitaifa.
Eagles tumefanikiwa kutunukiwa vyeti vya shule bora kwa muda wa miaka tatu mfululizo na kwa kipindi cha miaka tano.
Pia ni mara ya tatu kupata mwanafunzi bora kwenye 10 bora ya kitaifa” alieleza Mwenyekiti huyo wa Bodi.

Kwa upande wake Meneja wa shule hiyo, Bwana. George Fumbuka amewashukuru wazazi kwa kuwaamini na hivyo wataendelea kufanyia kazi mapungufu huku wakitarajia kuanzisha kozi zaidi shuleni hapo ili kuendana na matakwa ya Nchi. “Kwa sasa tunakuja kufundisha lugha za Kifaransa, kiarabu na Kichina. Mafunzo ya kilimo, Kareti, vipaji na muziki vyote hivi vitapatikana hapa Eagles” alisema Meneja huyo wa shule.

YouTube TV icon small
https://youtu.be/zpfbVnqSyx0

Aidha Mkuu wa shule hiyo, Bwana. Adam Myombe akisoma taarifa maalum ya mahafali hayo ya 10, alibainisha kuwa, moja ya dira ya Eagles toka kuanzishwa kwake mwaka 2006, ni kuwa shule inayoongoza kwa kutoa elimu bora ya sekondari kwa vijana ikiwaandaa kukabiliana na changamoto za kisayansi zinazoibuka pamoja na kuwa wachambuzi na watu wenye fikra huru.

“Mahafali haya ya 10 ya kidato cha nne mwaka huu, tunaadhimisha miaka 12 tangu kuanzishwa kwa shule hii huku ikikua na kuimarika siku baada ya siku katika harakati za kutimiza malengo yake.

Wetu wetu leo 71 wapo katika makundi matatu: Masomo ya sayansi wapo wahitimu (20), masomo ya sanaa wapo (23) na masomo ya biashara wapo (28).
Tunawaomba wajiunge na masomo ya kidato cha tano na sita ili waendelee kuipalilia njia katika kuelekea maisha ya kiuwajibikaji na yenye heri.” Alieleza Mkuu huyo wa shule.

Mwl wa IT Bi Janeth Mafuru akielezea mfumo huo kwa  Mgeni rasmi nk

Mwalimu wa Mfumo wa Mawasiliano (IT) Bi. Janeth Mafuru akielezea namna ya mfumo huo unavyofanya kazi kwa Mgeni rasmi na wageni mbalimbali wakati wa mahafali hayo ya 10 ya sekondari ya Eagles. Kushoto kwake ni Mkuu wa shule Bw. Adam Myombe.

Aidha, akielezea mfumo mpya waliouzindua utasaidia shule hiyo kwenda kisasa zaidi huku akiwapongeza watalaam wa kampuni ya Tanzania Experts Messrs Westfield Technologies Company Limited ambao waliandaa mfumo huo.

“Mfumo huu unaleta mabadiliko makubwa kwa shule katika namna ya kusimamia utoaji wa huduma za kitaaluma. Mfumo huu unawezesha mawasiliano huru kati ya walimu wa madarasa, utawala na wazazi, wote wakiwa na haki ya kufuatilia na kupata taarifa kulingana na mahitaji yao.” Alieleza Mkuu huyo wa shule.
Aidha aliipongeza kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) kwa kutoa ‘fast fibre-optic spectrum’ chini ya kauli mbiu yake ya “RUDI NYUMBANI KUMENOGA”.
“Tunaamini shule hii ni ya kwanza kupata mfumo huu kwa Bagamoyo na pengine nchini kote.

Nae Mwenyekiti wa kituo cha Maadili, Bwana Florentine Senya amewataka Wanafunzi hao kuelewa kuwa kwa sasa wanarudi kwa jamii hivyo wazingatie maadili walifundishwa shule.
“Hapa mpo 71 kama wahitimu wote. Mnamaliza kidato cha Nne wote kwa kuzingatia maadili bora mtasonga mbele kidato cha tano na sita na vyuo vikuu muwe salama.

Wazazi turudi kwenye malezi kwa sasa tuwasaidie kwenye malezi mema kama mlivyojilea nyie” alieleza Mwenyekiti huyo wa kituo cha Maadili.
Pia aliwataka wanafunzi waliobaki kuhakikisha wanaanzisha Klabu za maadili ili kujijengea uwezo wa kujitambua na kujikubali.
Bwana Senya amewataka wazazi na walezi waendelee kuwafundisha malezi bora watoto wao ambao kwa sasa wanarudi nyumbani huku akiwaachia swali: “Wazazi mnalea ama mnatunza?”.

Katika mahafali hayo, wanafunzi walipatiwa vyeti vyao vya kuhitimu huku wanafunzi wengine akitunukiwa vyeti kwa kuweza kufanya vizuri katika masomo yao ya taalum pamoja na mambo mbalimbali shuleni hapo.

Soma zaidi... ZanziNews